SHIRIKA la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) lipo katika hatua za mwisho zitakazowezesha Hifadhi ya Taifa ya Kitulo kupandikizwa aina mbalimbali za wanyamapori ili kuiongezea mvuto na kukuza shughuli za utalii nchini.
SHIRIKA la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) lipo katika hatua za mwisho zitakazowezesha Hifadhi ya Taifa ya Kitulo kupandikizwa aina mbalimbali za wanyamapori ili kuiongezea mvuto na kukuza shughuli za utalii nchini.
Kitulo ni hifadhi yenye zaidi ya spishi 350 za mimea jamii ya
frola zikiwemo aina 45 za maua ya porini ambayo yamewafanya wenyeji waiite
bustani ya Mungu huku wataalamu wa mimea wakiita Serengeti ya maua.
Pamoja na maua, hifadhi hiyo iliyopo wilayani Makete, mkoani
Njombe ina aina mbalimbali za ndege wanaohama kati ya hifadhi hiyo na Ulaya na
wanyama wengine jamii ya nyani wakiwemo Kipunji na kima.
Mhifadhi wa hifadhi hiyo, Fredrick Chuwa
aliwataja wanyama wanaotarajiwa kupandikizwa hifadhini humo kuwa ni pamoja na
Pofu, Pundamilia, Swala na wanyama jamii ya nyati.
Chuwa alisema tafiti mbalimbali
zinaonesha wanyama hao waliokuwepo katika hifadhi hiyo miaka mingi iliyopita na
wakapotea kwasababu mbalimbali ikiwemo ya ujangili.
“Mchakato wa kupandikiza wanyama hao unafanywa
kwa ufadhili wa Shirika la Uhifadhi Wanyamapori na Mazingira-WCS, na mambo
yakienda vizuri shughuli ya upandikizaji inaweza kuanza wakati wowote mwakani”
alisema.
Alisema mpango huo umekuja huku Mradi wa
Kuimarisha Maeneo ya Hifadhi Kusini mwa Tanzania (SPANEST) ukiendelea kuboresha
hifadhi hiyo.
Mratibu wa SPANEST, Godwell Ole
Meing’ataki alisema mradi huo ulioanza kutekelezwa mwaka 2012 kwa ufadhili wa pamoja
baina ya serikali ya Tanzania, Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP)
na Mfuko wa Dunia wa Mazingira (GEF) umejikita katika maeneo makubwa mawili.
Aliyataja maeneo hayo kuwa
ni ukanda wa Ruaha unaohusisha Hifadhi ya Taifa ya Ruaha, maeneo ya jumuiya za
hifadhi za wanyamapori ya Mbomipa na Umemarua, na mapori ya akiba ya Rungwa,
Muhesi na Kizigo.
Ukanda mwingine kwa mujibu
wa mratibu huyo, ni wa Kitulo-Kipengele unaohusisha Hifadhi ya Taifa ya Kitulo,
pori la akiba la Mpanga Kipengele, bonde la Numbe, na hifadhi ya mlima Rungwe
na Bujingijila.
Katika hifadhi ya Kitulo,
Meing’ataki alisema mradi umeshughulikia changamoto zake mbalimbali ikiwemo ya
kuboresha usimamizi wa hifadhi hiyo kwa kuweka alama za mipaka yake na kutoa elimu
ya uhifadhi na ulinzi kwa wananchi wanaozunguka hifadhi hiyo.
Alisema mbali na kutoa
mafunzo kwa askari wa hifadhi, mradi utaiwezesha hifadhi hiyo kufanya ulinzi
kwa kutumia mfumo wa mawasiliano wa kidigitali, teknolojia itakayofungwa mwaka
huu.
“Lakini pia tumetoa mafunzo
kwa askari wa hifadhi na kuongeza vifaa vya ulinzi likiwemo gari kwa ajili ya
doria,” alisema na kuongeza kwamba mradi pia umefanya utafiti wa kujua
kilichopo katika hifadhi hiyo kwa sasa.
No comments:
Post a Comment